Tamko la CEMOT kuhusu hali inayoendelea kujitokeza baada ya zoezi la kupiga kura.

Oktoba 26, 2015


Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar zikiendelea na zoezi la kuhesabu kura na kutangaza matokeo, Kituo cha Uangalizi wa Uchaguzi (CEMOT) kimepokea taarifa mbalimbali kutoka mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ndani na nje ya nchi zinazogusa mchakato wa uchaguzi. Baadhi ya taarifa hizo ni zifuatazo:

  1. Chama cha CUF kimeripotiwa kujitangazia ushindi wa Mgombea wao wa Uchaguzi wa Urais wa Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) chashinda uchaguzi wa kihistoria Zanzibar (“Civic United Front wins historic victory in Zanzibar election”).
  2. Taarifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Vyombo vya Habari, kuhusu siku ya kupiga kura, propaganda hatarishi, kauli za Ukawa za kutokubali matokeo, na ratiba ya mgombea wake wa Urais. 
  3. Taarifa zilizowekwa kwenye akaunti ya mjumbe wa kamati ya ushindi wa CCM, January Makamba, iliyosomeka “Dkt. John Pombe Magufuli kutangazwa Rais Mteule tarehe 29 Oktoba 2015”.
  4. Mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ushindi wa Mgombea wao wa Urais pamoja na idadi ya majimbo ambayo CCM kimeshinda.
  5. Taarifa rasmi ya kutoka UKAWA kuhusu uchaguzi mkuu, tarehe 25 Oktoba 2015. 
  6. Barua ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuhusu kukamatwa kwa maafisa mawasiliano wa mgombea wake wa Urais. 

Pamoja na kuheshimu uhuru wa taasisi na watu binafsi kutoa maoni yao, CEMOT inashauri kuwa katika kipindi hiki, kuna umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza mchakato wa uchaguzi, na kuepuka kauli zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Aidha, mamlaka husika zinayo dhamana ya kujibu tuhuma hizo mapema ili kuepusha malumbano na misuguano isiyo ya lazima.

CEMOT inawashauri wadau wote wa uchaguzi, waziachie Tume za Uchaguzi fursa ya kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na taratibu. Tunaomba wagombea pamoja na vyama vya siasa kuwaandaa wafuasi wao kupokea na kuheshimu matokeo ya uchaguzi. Pale ambapo wanakuwa na malalamiko, wayapeleke kwenye vyombo vya sheria.

CEMOT inawapongeza wananchi kwa utulivu walioonesha wakati wa zoezi la kupiga kura na Tume za Uchaguzi kwa kusimamia zoezi hilo. CEMOT inawahimiza wananchi kwa ujumla na wadau wengine wa uchaguzi kuendelea kuwa watulivu wakati Tume zinaendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi. Imetolewa na CEMOT
Hyatt Regency The Kilimanjaro Hotel, Dar es Salaam
Tarehe 26, Oktoba 2015

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger TemplatesPublished.. Blogger Templates