Ushiriki wa wanawake katika Uchaguzi wa 2015


Utangulizi

Ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi umebainishwa katika mikataba yote ya kimataifa, na kikanda ambayo Tanzania imeridhia, pamoja na kubainishwa katika sera na sheria za nchi. Kwa mfano, Mpango kazi wa Kimataifa Kuhusu haki za Wanawake (Beijing Platform of Action 1995) ulibainisha maeneo kumi na mbili ya kipaumbele, mojawapo likiwa ni ushiriki wa wanawake katika vyombo vyote vya maamuzi. Katika ngazi ya kikanda, Tamko la AU (AU Solemn Declaration) limeainisha lengo la ushiriki wa wanawake katika ngazi zote za maamuzi kwa asilimia 50/50 kufikia mwaka huu wa 2015, pamoja na Itifaki ya Maputo inayosisitiza usawa wa jinsia katika vyombo vya maamuzi. Vile vile Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ikiwa sheria mama ya nchi, pamoja na Katiba Pendekezwa (2014) zimelenga kujenga jamii yenye usawa, haki na huru. Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) inakiri kwamba ushiriki wa wanawake katika mfumo wote wa maamuzi ni mdogo kutokana na mila, desturi na tamaduni. Lengo la sera hii ni kutoa mwongozo wa kurekebisha upungufu huu wa kihistoria ili kuwezesha taifa kutekeleza azma ya kujenga jamii inayoongozwa na misingi ya usawa, haki na utawala wa sheria usiobagua.

Mwezi wa tisa mwaka huu, mataifa ya dunia yalikutana kubainisha malengo mapya ya kupewa kipaumbele miongo michache ijayo. Mh. Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alikiri mbele ya viongozi wenzake kwamba kati ya vipaumbele kumi na saba, usawa wa jinsia utapewa kipaumbele. Alikiri kwamba azma ya serikali ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ni kuweka uwiano katika nyanja zote za uongozi, pamoja na kubadilisha sheria zote zenye viashiria vya ubaguzi.

Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa kihistoria katika harakati za ushiriki wa wanawake katika chaguzi zote tangu tupate uhuru. Kwa mara ya pili, mwaka huu tumeshudia chama kimoja ACT-Wazalendo kumsimamisha mwanamke kwenye kiti cha nafasi ya urais, Mama Anna Mghwira. Vile vile kwa mara ya kwanza, chama tawala CCM, kimemteua mwanamke kama mgombea mwenza wa kiti cha Urais, Mama Samia Suluhu Hassan. Tunaweza kusema kuwa haya ni mafanikio makubwa katika nchi yetu.

Pamoja na mafanikio haya, idadi ya wagombea wanawake katika ngazi za ubunge na udiwani katika uchaguzi wa mwaka huu, haioneshi ongezeko. Katika ngazi ya udiwani uwiano ni mdogo zaidi.

Takwimu tulizozipata kutoka Tume ya Uchaguzi zinaonesha kwamba, wanaogombea nafasi ya urais ni nane, ambao ni wanaume 7 na mwanamke 1. Tofauti na miaka iliyopita wanawake walioonesha nia ya kuwania nafasi ya urais kwa chama tawala walikuwa saba. Wawili walifanikiwa kufika katika ngazi ya Mkutano Mkuu.

Idadi ya wagombea nafasi za Ubunge ni 1,235, wanawake ni 234 na wanume ni 1,001. Hii inammanisha kwamba wanaowania nafasi za uwakilishi katika Bunge la Muungano, wanawake ni asilimia 19% na wanaume asilimia 81%. Ikumbukwe kwamba wako wanawake wengi waliowania nafasi hizi lakini wakachujwa katika ngazi za awali. Katika nafasi za udiwani, uwiano umekuwa mbaya zaidi. Jumla ya wanaogombea nafasi za udiwani, ni 10,879, wanawake ni 679 au asilimia 6.2% tu.

Takwimu hizi hazitupi matumaini ya kufikia azma ya asilimia 50/50 kama Mh. Rais Kikwete alivyokiri mbele ya mataifa mengine na kama ilivyobainshwa katika mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania.

Ukilinganisha takwimu za ushiriki wa wanawake kama wagombea na takwimu za uchaguzi wa 2010, utaona kwamba hakuna mabadiliko. Waliogombea nafasi za ubunge wa Jamhuri ya Muungano walikuwa 1,036, wanawake wakiwa 191 tu, sawa na asilimia 18%. Hii inamaanisha kwamba, pamoja na matamko yote na harakati za wanawake za kudai usawa katika ngazi hii ya uwakilishi, kumekuweko na ongezeko la asilimia 1% tu la wanawake wanaogombea nafasi hizi za ubunge. Takwimu hizi, ni kiashiria kwamba kazi ya kuweka mfumo mbadala utakaoweza kujenga misingi ya usawa wa jinsia bado ni kubwa, na kwamba jitihada za makusudi zinatakiwa ili kuleta mabadiliko ndani ya vyama.

Kuna vikwazo vingi vinavyoendelea kukwamisha ushiriki wa wanawake katika kuwania nafasi za uongozi. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mtizamo kwamba wanawake hawana uzoefu, na mfumo wa uchaguzi ambao hauweki misingi ya usawa katika uwakilishi. Kuna mwendelezo wa tamaduni zilizojikita kwenye “mfumodume”, na taratibu zinazoweka vikwazo katika safari ya uongozi kwa wanawake. Pia, kuna ukatili wa jinsia katika chaguzi. Vyama vya siasa havijaweka nia ya kuleta mabadiliko ya mfumo wa uongozi ndani ya vyama vyao. Maamuzi mengi kuhusu ushiriki wa wanawake katika uchaguzi yanafanywa na vyama vinaovyoongozwa na “mfumodume”.Takwimu na taarifa mbalimbali za uchaguzi, zikiwemo za NEC pamoja na za waangalizi wa uchaguzi, zinatupa taswira ya ushiriki wa wanawake katika uchaguzi wa mwaka huu.

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger TemplatesPublished.. Blogger Templates