Kwanini Wagombea wa Urais wa CCM na Chadema wamekwepa Mdahalo kwa Luninga?


Na Ruth Meena 

Midahalo ya wagombea wa nafasi ya urais kwa njia ya luninga huwezesha wanaoomba kura kukabiliana na maswali ya wapiga kura ili waweze kuelezea na kutetea sera zao kama zilivyobainishwa kwenye ilani za vyama vyao. Tofauti na mikutano ya hadhara ambapo wagombea wanaeleza sera zao na kuomba kura, mdahalo huwezesha wapiga kura kuhoji sera na ahadi za wagombea na kuwapa wagombea nafasi ya kufafanua mambo yaliotokana na hotuba zao katika mikutano ya kampeni. Hapa kwetu utamaduni wa kuwa na midahalo ya wagombea haujazoeleka sana kama sehemu ya kampeni. Katika uchaguzi wa mwaka 2010,
wagombea wa chama tawala walikataa kushiriki kwa sababu ambazo hazikuelezwa wazi. Mwaka huu, pamoja na mgombea wa CCM kukubali kushiriki, baadaye alijitoa huku mgombea kwa tiketi ya UKAWA alikataa toka mwanzo kuwa asingeshiriki mdahalo huo. Ni sababu zipi zinazofanya wagombea hususani wa vyama vyenye
nguvu kukataa kushiriki katika midahalo ya luninga? 

CCM na UKAWA wamekuwa wakichukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari hasa kurasa za mbele za magazeti, au habari kuu kwenye redio na luninga. Kwa maneno mengine, wao walionekana wazoefu wa habari. Iweje basi wakatae kushiriki kwenye mdahalo?
Kampeni za wagombea hawa wawili hazitofautiani sana kwenye masuala ya misingi, itikadi, au sera mbadala za kubomoa mifumo kandamizi. Nahisi, hofu kubwa ya hawa wagombea wawili ni: kwanza, totauti zao za kiitikadi hazijabainishwa. Pili, msimamo wao kuhusu mfumo dume, na mifumo kandamizi hazijajitokeza. Tatu, msimamo wao kuhusu msingi wa kuwezesha ukuaji wa uchumi linganifu haujajitokeza. Nne, hofu ya kwamba, endapo vyama vidogo ambavyo havijapata nafasi kubwa ya kunadi sera zao mbadala vikifanya vizuri, na hasa kuweza kuwavutia vijana na wanawake, vingeliweza kubadilisha mawazo ya baadhi ya wapiga kura dakika hizi za majeruhi. Kukwepa mdahalo kunatupa sisi wapiga kura wasiwasi kama kweli ahadi zinazotolewa kwenye majukwaa zinataweza kubomoa mfumo, na kama kuna nia ya dhati ya kuleta mfumo mbadala.

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger TemplatesPublished.. Blogger Templates