TAARIFA YA AWALI
UTANGULIZI
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni uchaguzi wa tano tangu Tanzania tuliporejea kwenye mfumo wa vyama vingi. Uchaguzi huu unafanyika kwa kuzingatia Katiba za Jamhuri ya Muungano (1977) na Katiba ya Zanzibar 1984 toleo la 2010 pamoja na sheria zinazosimamia uchaguzi za pande zote mbili. Uchaguzi mkuu unahusisha kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge, madiwani, Rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa kuzingatia mfumo wa kisheria kwa pande zote za muungano, mchakato wa uchaguzi unaongozwa na Tume ya taifa ya Uchaguzi (kwa muungano) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (kwa upande wa Zanzibar). Tume hizi zina mamlaka ya kisheria kusimamia zoezi zima la uchaguzi kuanzia kutoa elimu ya mpiga kura, usajili wa wapiga kura, ugawaji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi, upigaji kura, ukusanyaji na utangazaji wa matokeo.
Tanzania imeridhia mikataba mbali mbali ya kimataifa inayohusu uchaguzi ikiwa ni pamoja na Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa; mkataba wa Afrika juu ya Demokrasia, uchaguzi, na utawala; na mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki juu wa utawala bora. Kwa kuzingatia mikataba hii, Tanzania imekuwa ikialika waangalizi kutoka pande mbali mbali za dunia kushuhudia mchakato wake wa uchaguzi.
Uangalizi wa uchaguzi kwa kupitia waangalizi wa ndani unaendelea kuwa eneo la umuhimu wa pekee kwenye michakato ya uchaguzi yenye kuzingatia uadilifu na uwazi kote barani Afrika. Hii inatokana na ukweli ulio dhahiri juu ya maslahi ya moja kwa moja ya waangalizi husika ambao si tu ni raia lakini pia ni wakazi wa nchini na kwenye maeneo uangalizi unapofanyika. Kwa kutambua hili, wana nafasi ya pekee katika kuangalia na kukusanya taarifa za uhakika kuhusu michakato ya uchaguzi.
Utaratibu wa uangalizi wa uchaguzi kwa kutumia mfumo wa kituo cha uangalizi wa uchaguzi (Election Situation Room) ni mfumo unaowezesha asasi za kiraia zinazoshiriki kwenye uangalizi wa uchaguzi kukusanya taarifa kwa haraka na kutoa fursa kwa wale wanaosimamia mchakato wa uchaguzi kushughulikia masuala yanayoibuka kwa haraka na kwa wakati. Mfumo huu unaotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na mifumo ya kidijitali unategemea ushirikiano kati ya wadau husika ili kupata matokeo bora. Uwepo wa taarifa za uhakika kutoka kwa waangalizi na uwezo wa kuzitathmini taarifa hizo kwa haraka kunatoa fursa ya ushirikiano mpana kati ya waangalizi na wasimamizi wa mchakato wa uchaguzi. Mfumo huu unajitofautisha na utaratibu uliokuwapo awali wa kuangalia uchaguzi na kutoa tathmini mwisho wa mchakato na hivo kupunguza uwezekano wa kushugulikia masuala yanayoibuka kwa uharaka.
Kwa ufupi Kituo cha Uangalizi wa Uchaguzi kililenga kutimiza malengo yafuatayo:
Kukusanya taarifa juu ya matukio muhimu yanayohusu mchakato wa uchaguzi kutoka majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima
Kufanya tathmini ya taarifa zinazopokelewa juu ya mchakato mzima kwa lengo la kuchangia kuuboresha kwa wakati
Jumla ya waangalizi 10,050 walisambazwa kwenye majimbo yote ya uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi
Taarifa nyingine zilikusanywa kutoka vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kutathiminiwa na kuhakikiwa kulingana na aina ya taarifa.
Kwa muktadha huo, Muungano wa Waangalizi wa ndani yaani Coalition on Election Monitoring and Observation in Tanzaina (CEMOT) ulifuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi na kubainisha matukio ya pekee katika kipindi cha mchakato huu, ulitathmini madhara ya mienendo inayoonekana na matukio yanayoibuliwa na waangalizi na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha imani ya umma na uadilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Uangalizi wa uchaguzi wa mwaka 2015 unaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), katiba ya Zanzibar (1984 toleo la 2010), Sheria za uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano (1985), sheria ya uchaguzi Zanzibar (2010), Mkataba wa Afrika juu ya Demokrasia, Uchaguzi na Utawala, vyombo na mikataba ya kimataifa pamoja na taratibu na utamaduni uliokubalika kufikia uchaguzi wenye uadilifu.
Kwa kuzingatia haya uangalizi huu unatathmini uadilifu wa mchakato wa uchaguzi unaoheshimu misingi ya kidemokrasia kwa kutilia maanani vigezo vifuatavyo:
Ushiriki usio na vizingiti kwa wote wanaostahili
Usawa wa fursa za ushiriki kwa wote wanaoshiriki kwenye mchakato wa uchaguzi
Weledi, uwazi na kutokuwa na upendeleo kwenye maandalizi na usimamizi wa mchakato wa uchaguzi
Uangalizi huu ulizingatia tathimini za nyuma za uchaguzi mkuu uliopita (2010) na ripoti za waangalizi mbali mbali. Kwa kuzingatia mikataba, sharia, kanuni na taratibu husika uangalizi wetu ulitazama mambo yafuatayo:
Ushiriki na ushirikishwaji bila kikomo wa wote wanaostahili
Haki na fursa ya wote wanaostahili kushirki kupiga kura
Haki na fursa ya wote wanaostahili kuchaguliwa
Uwazi wa vyombo vya usimamizi wa uchaguzi
Uwajibikaji wa vyombo vya usimamizi wa uchaguzi
Mfumo na utaratibu wa kutatua vikwazo mbali mbali vya ushiriki katika mchakato wa uchaguzi
Waangalizi walijikita zaidi kuangalia mchakato wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura na kutangazwa kwa matokeo. Kwa ufupi, waangalizi wetu wameshuhudia yafuatayo:
Vyama na wagombea wamepata fursa ya kushiriki na kushirikishwa bila vikwazo katika mchakato wa uchaguzi ingawa wanachi wachache waliostahili kupiga kura wamepoteza fursa hiyo kwa majina yao kutoonekana katika daftari
Wagombea na vyama wamepata fursa kubwa ya kushiriki kwenye mchakato mzima ingawa wanawake bado wameachwa nyuma.
Tume zimejitahidi kutimiza wajibu wake na zinahitaji kuwajibika zaidi kwa wadau na umma katika hatua zote za uchaguzi.
Mfumo wa malalamiko na rufaa wa tume unastahili kuendelea kuimarishwa
Katiba na sheria za nchi ndio msingi wa suluhu wa migogoro inayoibuka katika mchakato huu
UADILIFU WA MCHAKATO WA UCHAGUZI
Mnamo tarehe 25/10/2015, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Uchaguzi mkuu wa tano tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992. Uchaguzi wa Rais, Mbunge na Diwani kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniaulifanyika sambamba na ule wa Rais wa Zanzibar na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kulikuwa na wagombea 8 wa nafasi ya Urais (mwanamke 1), wagombea 1250 wa nafasi ya ubunge (wananwake 238) na wagombea udiwani wapatao 10,879 nchini kote. Nafasi ya Urais Zanzibar iligombaniwa na vyama 14 vikiwemo vyama vyenye upinzani mkali CCM na CUF.
Katika kutathmini mchakato wa uchaguzi tuliangalia viashiria vitatu. Kwanza kabisa tuliangalia kama mchakato wa uchaguzi ulizingatia msingi wa usawa kwa makundi yote katika jamii: haki ya kupiga kura, haki ya kuchaguliwa na haki ya kupata taarifa. Pili, tuliangalia uwazi wa mchakato wa uchaguzi, haki ya wapiga kura kupata taarifa sahihi kuhusu mchakato wa uchaguzi, haki zao wakati wa uchaguzi na haki za kupata taarifa za wagombea. Tatu, tuliangalia uwajibikaji kwa mamlaka zinazosimamia uchaguzi. Hapa tuliangalia uwajibikaji wa mamlaka zinazosimamia uchaguzi, ufanisi katika kutoa maamuzi yahusianayo na ukiukwaji wa kanuni na taratibi za uchaguzi, pamoja na kuchukua hatua za kisheria kuhusu makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
HAKI YA KUCHAGUA NA KUCHAGULIWA
Takwimu zitonakanazo na Ofisi za Takwimu za Taifa(NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar ilikadiriwa kwamba, ifikapo wakati wa uchaguzi Tanzania ingekuwa na idadi ya watu wapatao 48,522,228, kati ya hao, wenye sifa za kupiga kura walikadiriwa kufikia 24,252, 541. Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguxi za zinaonyesha idadi ya watu waliondikishwa kwenye daftari la wapiga kura kuwa ni 23,553,982 - Tanzania Bara watu 22,750,789 na Zanzibar watu 503,193. Hii inamaanisha kwamba 95.9% ya wenye sifa za kupiga kura waliandikishwa. Kati ya walioandikishwa kwenye daftari la wapiga kura Tanzania Bara wanawake ni 11,950, 200 sawa na53% ya wapiga kura wote. Mchanganuo wa walioandikishwa kwenye daftari la mpiga kura unaonyesha kuwa vijana wenye umri 18-35 ni 12,894 576(57%) kati yao wanawake ni 6,738,964. Watu wenye umri 36-50 ni 5,690,668 (25%) kati yao wanawwake ni 2,946,247, na miaka 50+ ni 4,165,544 (18%) ambapo wanawake ni 2,264,990. Uandikishwaji ni hatua ya awali ya kuwezesha wapiga kura kutumia haki yao ya kuchagua viongozi na wawakilishi katika ngazi mbambali za kufanya maamuzi.
HAKI ZA KUCHAGULIWA
Vyama vya siasa nchini vina madaraka makubwa ya kuamua nani atakayeteuliwa kuwa mgombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi. Kwa vyama vingi kanuni na taratibu za uteuzi haziko wazi. Hali hii inatia dosari katika ya kutekeleza matakwa ya demokrasia ndani ya vyama vya siasa. Sheria ya vyama vya siasa haiviwajibishi vyama vya siasa kuweka au kufuata utaratibu wa kuwezesha ushiriki sawa wa wanawake na makundi mengine katika kuteua watu walioonesha nia ya kuwania viti vya uwakilishi katika uchaguzi.
UTEUZI WA WANAWAKE
Idadi ya wagombea nafasi za Ubunge ni 1,250, wanawake ni 238. Hii inammanisha kwamba kati ya waliowania nafasi za uwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanawake walikuwa asilimia 19% tu ya wagombea. Ikumbukwe kwamba wako wanawake wengi wenye sifa waliowania nafasi hizi lakini wakachujwa katika ngazi za awali. Katika nafasi za udiwani, uwiano umekuwa mbaya zaidi. Jumla ya wanaogombea nafasi za udiwani, ni 10,879, wanawake ni 679 au asilimia 6.2% tu.
Ukilinganisha takwimu za ushiriki wa wanawake kama wagombea na takwimu za uchaguzi wa 2010, utaona kwamba hakuna mabadiliko. Waliogombea nafasi za ubunge wa Jamhuri ya Muungano walikuwa 1,036, wanawake wakiwa 191 tu, sawa na asilimia 18%. Hii inamaanisha kwamba, pamoja na matamko yote na harakati za wanawake za kudai usawa katika ngazi hii ya uwakilishi, kumekuweko na ongezeko la asilimia 1% tu la wanawake wanaogombea nafasi hizi za ubunge. Takwimu hizi, ni kiashiria kwamba kazi ya kuweka mfumo mbadala utakaoweza kujenga misingi ya usawa wa jinsia bado ni kubwa, na kwamba jitihada za makusudi zinatakiwa ili kuleta mabadiliko ndani ya vyama.
Kuna vikwazo vingi vinavyoendelea kukwamisha ushiriki wa wanawake katika kuwania nafasi za uongozi. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mtizamo kwamba wanawake hawana uzoefu, na mfumo wa uchaguzi ambao hauweki misingi ya usawa katika uwakilishi. Kuna mwendelezo wa tamaduni zilizojikita kwenye “mfumodume”, na taratibu zinazoweka vikwazo katika safari ya uongozi kwa wanawake. Pia, kuna ukatili wa jinsia katika chaguzi. Vyama vya siasa havijaweka nia ya kuleta mabadiliko ya mfumo wa uongozi ndani ya vyama vyao. Maamuzi mengi kuhusu ushiriki wa wanawake katika uchaguzi yanafanywa na vyama vinaovyoongozwa na itikadi ya ubaguzi.
Wagombea Ubunge Wanawake
Chanzo: NEC
Mchanganuo wa takwimu hizi kichama unatupatia picha hii: idadi ya wanawake wagombea nafasi za Bunge la Jamhuri Ya Muungano ni: wa CCM ni 9%, CHADEMA ni 6%, ACT Wazalendo 15%, CUF ni 11%na vyama vingine ni 36%. Hali hii ikiachwa iendelee bila hatua za kisheria, itachukua Tanzania miaka 155 kufiki lengo la 50/50 kama lilivyoainishwa kwenye itifaki ya Maputo, Tamko la AU, na Katiba pendekezwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uwiano katika nafasi za udiwani ni mbaya zaidi. Idadi ya wagombea katika nafasi hii ni 10,879, wanawake ni 679 au 6.2%. Hali hii ikiendelea hivi bila shuruti za sheria itachukua Tanzania miaka 150 au chaguzi 31 kwa vipindi vya miaka mitano mitano. Baadhi ya changamoto zinazokwamisha wanawake kwenye ushiriki ni pamoja na vyama kutokuwa na mikakati au nia ya kuzingaia misingi ya usawa, udhalilishwaji wakati wa kampeni, na ukosefu wa rasilimali za kampeni. Hata hivyo ripoti za waangalizi wa CEMOT zilizofanywa kwa siku sita kutoka kwa waangalizi 196, zinaonyesha kuwepo kwa taarifa chache za kudhalilisha. Takribani 5% ya wachunguzi walikiri kusikia suala la rushwa ya ngono, 9% walikiri kusikia matumizi ya lugha ya kudhalilisha, ambapo 2% walikiri kusikia kuumizwa kwa wagombea kimwili, ambapo 2% walisikia kukamatwa kwa wagombea bila sababu.
USHIRIKI WA VIJANA
Wapiga kura wenye umri kati ya miaka 18-35 ni 12,894, 576 au 57% ya wapiga kura wote. Kati yao wanawake ni 6,738964, na wanaume ni 6,155613. Kundi hili limeonekana kama turufu ya ushindi kwa vyama yote. Hakuna takwimu zinazoonesha wagombea kwa umri, hata hivyo vyama vingi viliwatumia vijana kama nguvu kazi kubwa katika shughuli za kampeni. Wagombea wote wa nafasi za urais na ubunge zimegusa mahitaji ya vijana kama vile ajira, elimu ya bure, mafunzo ya ufundi na kuwawezsha kisiasa. Pamoja na kutegemea vijana kama nguvu kazi, inaonekana vijana wamekuwa wahanga wa vurugu zilizotokea kwenye maeneo machache, kwa mfano vijana wa CHADEMA 191, wamekamatwa na vyombo vya dola kwa tuhuma ambazo hazijatamkwa rasmi na hadi leo hii bado wanashikiliwa na polisi.
USHIRIKI WA WATU WENYE ULEMAVU
Takwimu za idadi ya watu na makazi zinaoonyesha kwamba takribani 5.8 % ya Watanzania ni wenye kuishi na ulemavu. Hata hvyo takwimu hazioneshi idadi ya watu wenye ulemavu wenye sifa za kupiga kura. Watu wenye ulemavu wa kuona walitayarishiwa karatasi za kupiga kura kwa nukta nundu. Hali hii iliwezesha kundi hili kutumia haki yao ya kupiga kura ya siri pale ambapo karatasi hizi zilifikishwa. Taarifa kutoka kwa waangalizi wa CEMOT wapatao 1,736 waliotoa taarifa kuhusu kuwepo kwa kwa karatasi za maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watu wenye wenye ulemavu wa kuona, 48% walikiri kuwepo kwa karatasi za nukta nundu ambapo 52% walisema hapana (hata hivyo huenda wale walionesema hapana ilitokana na kutokuwepo kwa watu wenye ulemavu huu).
UFANISI NA WELEDI WA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI
Wadau wakuu kwenye kutekeleza mchakato wa uchaguzi
Kazi kuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni pamoja na kuratibu wadau wa uchaguzi na kusimamia shughuli zote zihusianazo na mchakato wa uchaguzi - yaani kabla ya uchaguzi, wakati wa kupiga kura, kutoa tamko rasmi la matokeo, kuchambua mchakato na kuanza mchakato wa uchaguzi unaofuata.
Wajibu wa Tume za Taifa Uchaguzi
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (1977) Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepewa majukumu yafuatayo;
Kusimamia na kuendesha Uandikishaji wa Wapiga Kura kwaajili ya Uchaguzi wa Urais, Ubunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais na Ubunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupitia mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo mbali mbali ya Uchaguzi wa Ubunge.
Kusimamia na kuendesha Uandikishaji wa Wapiga Kura na kuendesha Uchaguzi wa Madiwani.
Kutangaza matokeo ya Viti Maalum vya wanawake vya Ubunge na Udiwani.
Kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kusimamia Watu na Asasi zitazokazohusika katika Kutoa Elimu hiyo.
Kutekeleza Majukumu mengine yatokanayo na sheria zilizotungwa na Bunge.
Uandikishaji
Kwa mara ya kwanza, Tanzania imetumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura kwa njia ya Biometric. Mfumo huu ukitumika vizuri unarahisisha kumtambua mpiga kura, na kuzuia uwezekano wa watu kupiga kura mara nyingi. NEC iliwezesha uandikishaji watu wenye sifa yakupiga kura takriban 95.6%. Tume inastahili pongezi kwa mafanikio haya makubwa hasa ikizingatiwa mazingira magumu Tume iliyokabiliana nayo wakati wa zoezi la uandikishaji ikiwemo ufinyu wa rasilimali fedha na uhaba wa vifaa vya uandikishaji (BVR kits).
Elimu ya wapiga kura
Elimu ya Wapiga Kura ni muhimu sana kuwezesha wapiga kura kutumia haki yao ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa. Wadau wanaotoa elimu hii ni pamoja na Tume za uchaguzi, vyama vya siasa na asasi za kiraia. Ripoti za waangalizi wa CEMOT zilionesha kwamba elimu ya mpiga kura ilitolewa kwa kiasi kidogo japo kasi ya utoaji wa elimu hiyo iliendelea kuongezeka zaidi kwa kadri muda kuelekea siku ya uchaguzi ulivyoendelea kukaribia. Mchoro huu unaonesha.
Maandalizi ya Uchaguzi
Taarifa hizi zinatokana na ripoti 3,657 kutoka kwa waangalizi 301, kati ya tarehe 25 Septemba hadi tarehe 22 Oktoba.
Waangalizi waliotoa taarifa kuhusu hali ya matayarisho ya uchaguzi mkuu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa orodha ya wapiga kura vituoni hadi kufikia tarehe 22/10/2015, siku tatu kabla ya uchaguzi mkuu. Jumla ya maeneo 3,657 yalitembelewa na waangalizi 301 na kubaini yafuatayo: Waangalizi wameripoti kushuhudia orodha za wapigakura kubandikwa kwenye 55% ya maeneo (vituo) vilivyotembelewa.
waangalizi Asilimia 55% wameshuhudia vyama kupewa taarifa za vituo vya kupiga kura
Asilimia 58% ya waangalizi wameona tangazo rasmi la uchaguzi
Kielelezo hapa chini kinaonyesha jinsi hali ya maandalizi kwa uchaguzi mkuu ilivyokuwa ikiboreka kuelekea siku ya uchaguzi.
Uratibu wa Kampeni
Tume ilipanga ratiba ya wagombea wa urais, na kusimamia utekekezaji wake. Pale ilipobidi tume iliweza kujadiliana na vyama na kutoa uongozi. Wakati mikutano ya vyama viwili ilipoingiliana kwenye matumizi ya viwanja vya Jangwani, TUME ilitoa uongozi kwa kutumia busara. .
Kwa ujumla, waangalizi hawakushuhudia vikwazo vingi vilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi au Jeshi la Polisi kwa ushiriki wa vyama na wagombea kwenye kampeni.
KUSIMAMIA KUPIGA KURA, KUTANGANZA MATOKEO
3.7.1 Kufungua vituo vya kupigia kura
Taarifa za waangalizi wa uchaguzi zinaonesha kuwa vituo vingi vilifunguliwa kwa wakati na upigaji kura ulianza kwa muda ulioainishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. Kati ya vituo 6,444 vilivyoangaliwa wakati wa ufunguzi, vituo 6,080 (94%) upigaji kura ulianza kwa wakati (Tazama kielelezo).
Chanzo: Taarifa za CEMOT
Taarifa pia zinaonesha kuwa vituo vyote vilivyoangaliwa wakati wa ufunguzi vilikuwa na Maafisa wa Uchaguzi wasiopungua watatu (3).
3.7.2 Uwepo wa vifaa vya kupigia kura na rasilimali watu
Taarifa za waangalizi wa CEMOT vituo 5,921 (90%) kati ya vituo 6,579 vilivyoangaliwa vilikuwa na vifaa vya kutosha. Vituo 658 (10%) vilikuwa na upungufu wa vifaa hasa mihuri.
Mambo mengine yaliyoangaliwa na waangalizi wa uchaguzi wa CEMOT ni pamoja na:
Vituo 1,224 (18%) kati ya vituo 6,579 kulikuwa na baadhi ya majina ya wapiga kura waliojiandikisha yaliyokosekana katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura;
Vyama vyote vilikuwa na fursa ya kuweka mawakala kwenye vituo vya kupigia kura. Taarifa 6,579 zilizowasilishwa CEMOT zinaonesha kuwa CCM ilikuwa na mawakala kwenye vituo 6,475 (98%), CHADEMA na vyama washirika vituo 6,351 (97%), na vyama vilivyobakia vituo 4,585 (70%);
Vituo 6,259 (95%) vilivyoangaliwa vilikuwa na ulinzi wa askari polisi wenye sare;
Vituo 6,075 (92%) vilifikika kwa urahisi na watu wenye changamoto za ulemavu.
MWENENDO WA UPIGAJI KURA
Taarifa ya mwenendo wa upigaji kura inatokana na ripoti za waangalizi kwenye vituo 5,770 vya kupiga kura, hadi saa moja na nusu jioni, siku ya uchaguzi, tarehe 25/10/2015
Taarifa zinaonesha kuwa uhakiki wa vitambulisho vya wapiga kura kwa kutumia daftari la kudumu la wapiga kura ulishuhudiwa kwenye vituo 5736 (99%) kati ya vituo 5,770 vilivyoangaliwa.
Taarifa zimeonesha kuwepo kwa dalili za kampeni ikiwa ni pamoja na vifaa vya kampeni karibu na vituo vya kupiga kura kwenye vituo 245 (4%) tu kati ya vituo 5,770.
Ukaguzi wa vidole ili kubaini kama vina alama za wino usiofutika ili kujiridhisha kuwa mpiga kura hajapiga kura mahali pengine ulishuhidiwa ukifanywa na maafisa wa uchaguzi katika vituo 5,161 (89%) vilivyoangaliwa. Aidha waangalizi walishuhudia wapiga kura wakichovya vidole kwenye wino maalumu usiofutika kwa urahisi kwenye vituo 5,680 sawa na 98% ya vituo vilivyoangaliwa. Taarifa za waangalizi zinaonesha kuwa watu wasiohusika walioruhusiwa kuingia katika kituo cha kupiga kura walishuhudiwa kwenye vituo 244 (4%) kati ya vituo 5,770 vilivyoangaliwa.
Taarifa za waangalizi wa Uchaguzi zinaonyesha kuwa kwenye vituo 2,492 (43%) kulikuwa na watu kwenye mistari wakisubiri kupiga kura ilipofika saa kumi kamili jioni. Mpiga kura wa mwisho alipiga kura kati ya saa 11.00 na saa 11.30 jioni katika vituo 824 (14%) kati ya vituo 5770 vilivyoangaliwa.
Kuhesabu Kura
Taarifa hizi zinatokana na ripoti za waangalizi kwenye vituo 5,325 vilivyoangaliwa hadi saa tatu asubuhi siku baada ya Uchaguzi.Vituo 2206 sawa na 41% kati ya vituo vya kupiga kura 5,325 vilianza zoezi la kuhesabu kura mara tu baada ya kumaliza upigaji kura saa 10.00 jioni. Vituo 1280 (24%) zoezi la kuhesabu kura lilianza kati ya saa 10.30 na saa 11.00 jioni. Vituo 1836 vilivyosalia vilianza zoezi hilo baada ya saa 11.00 jioni. Watu wasioruhusiwa kuwa katika vituo vya kuhesabia kura walishuhudiwa kwenye vituo 112 sawa na 2% ya vituo vilivyoshuhudiwa.
Waangalizi walishuhudia baadhi ya mawakala wa vyama katika vituo 561 (11%) vya kuhesabu kura ambao hawakukubaliana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na hawakuweka saini. Baadhi ya mawakala katika vituo 471 (9%) walitaka kurudiwa kwa zoezi la kuhesabu kura.
Waangalizi walishuhudia matokeo ya uchaguzi yakibandikwa nje ya vituo vya kupigia kura kwa nafasi mbali mbali kama ifuatavyo: Urais vituo 5013 (94%), Ubunge vituo 4,887 (92%), na Udiwani vituo 5038 (96%). Vituo 2309 (43%) vilibandika matokeo yote ndani ya nusu saa baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura; vituo 1483 (28%) vilibandika kati ya nusu saa na saa moja ambapo vituo 1533 (29%) ilichukua zaidi ya saa moja kubandika matokeo baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabu kura.
Tumeshuhudia taarifa za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo katika majimbo kama Mbagala, Kinondoni, Ubungo, Kibamba, Kawe, Mbozi, Iringa Mjini, Temeke, Ilala, Simanjiro, Babati, Nyamagana, Ukonga, Segerea, Shinyanga Mjini. Kwenye baadhi ya meneo haya ucheleweshaji umesababisha uvunjifu wa amani, majeruhi na uharibifu wa mali. Tunaamini vurugu hizi zingeweza kuepukika kama wasimamizi wa uchaguzi wa maeneo husika wangehakikisha upatikanaji wa haraka wa taarifa zote zinazohusu uhesabuji wa kura. Ni haki ya wananchi kujulishwa taarifa za muhimu kuhusu mchakato, aidha matokeo au sababu za kuchelewa kutolewa kwa matokeo.
Kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar na malalamiko yaliyoibuliwa na washindani wa uchaguzi huu yanahitaji maelezo fasaha toka kwa mamlaka husika kwa wakati muafaka. Tunaamini kuzingatia sheria na taratibu zilizopo Tume za Uchaguzi zina uwezo wa kushauriana na wadau wote wa mchakato wa uchaguzi huu kufikia maafikiano na makubaliano yatakayotuacha kama taifa moja lenye amani.
MAPENDEKEZO NA HITIMISHO
Kwa kuzingatia vigezo vya uangalizi wa uchaguzi tulivyovitumia, pamoja na mapungufu yaliyojitokeza, mchakato wa Uchaguzi Mkuu ulikwenda vizuri hasa katika hatua ya kampeni na upigaji kura ulioshuhudiwa na waangalizi wetu waliokuwepo nchi nzima.
Vyama na wagombea walipata fursa ya kushiriki na kushirikishwa bila vikwazo katika hatua za kampeni. Wananchi waliostahili kwa ujumla walipata haki na fursa ya kushiriki kwenye kampeni na kupiga kura bila vikwazo vingi. Hata hivyo wapo wananchi walioshindwa kushiriki kupiga kura kutokana na majina yao kutokuwepo katika daftari la wapiga kura. Tunaamini dosari hizi zitapata fursa ya kurekebishwa kabla ya chaguzi zijazo na Tume kupewa muda wa kutosha kuhakiki Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Hatujashuhudia vikwazo vingi vikiwekwa dhidi ya wagombea wa nafasi mbalimbali japokuwa kumekuwa na matukio machache ya kushambuliwa na kudhalilishwa kwa baadhi ya wagombea na maafisa wa Tume. Hata hivyo ushiriki wa wanawake umeendelea kuwa suala linalohitaji mkakati mahususi.
Tume zimejitahidi kutimiza wajibu wake kwa kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa kushirikisha wadau mbalimbali na umma kupitia vyombo vya habari. Katika ngazi za chini za usimamizi, tunaamini Tume kupitia kwa watendaji na wakala wake inastahili kuwajibika zaidi na kuimarisha uwazi ambao ni nyenzo muhimu katika kudumisha imani ya umma kwa mchakato. Uwazi huu unaweza kuimarishwa kwa ushirikishwaji mkubwa zaidi wa wadau hasa kupitia vyombo vya habari katika kupeana taarifa zote za msingi kuhusu mchakato wa uchaguzi.
Kwa kuzingatia majukumu ya Tume za Uchaguzi, mfumo wa malalamiko na rufaa kwa ngazi zote za uchaguzi unahitaji kuimarishwa ili kuhakikisha mapungufu yanayoibuka yanapata suluhu kwa haraka iwezekanavyo. Tunaamini utatuzi wa mapungufu hayo una nafasi ya pekee katika kupunguza manung’uniko na kuongeza imani si tu kwa Tume bali kwa mchakato mzima wa uchaguzi.
Ili kuepukana na sintofahamu inayoweza kusababisha kuvurugika kwa imani ya umma na amani ya nchi yetu, mamlaka husika hazina budi kuendelea kushirikisha wadau wote wa mchakato wa uchaguzi. Tume inastahili kusimamia majukumu yake kulingana na sheria zinazoziunda ili kuepukana na migogoro na manung’uniko yanayoweza kuathiri mchakato mzima.
Katiba na sheria za nchi ndizo zinazoweza kutoa suluhisho la uhakika la migogoro mingi inayoibuka katika kipindi hiki cha uchaguzi. Hata hivyo uchaguzi ni mchakato wa kisiasa ambao inapobidi hekima, busara na subira huhitajika ili kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake.
No comments: