na Ruth Meena
Tume za uchaguzi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar (ZEC) ni wadau wakuu katika uchaguzi. Zinawajibu mkubwa wa kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazohusu uchaguzi. Kimantiki shughuli za uratibu wa uchaguzi zinaweza kuathiri sana matokeo ya uchaguzi hususani katika suala la kujiandikisha kupiga kura, kuendesha kampeni, kusimamia maadili ya vyama vya siasa na wagombea wao, pamoja na kusimamia upigaji kura. Aidha katika utelezaji wa shughuli zake Tume ina nafasi kubwa ya kuathiri ushiriki wa wanawake na makundi yaliyoko pembezoni.
Kwa mujibu wa sheria, Tume hutoa miongozo na kusimamia utekelezaji wake kwa wadau wote wa uchaguzi. Baadhi ya miongozo ni ya kuelekeza wachunguzi wa ndani na wa nje na kutoa masharti ya uchunguzi na mambo ya kuchunguza, pamoja na kubainisha haki zao. Tume ya Uchaguzi ya Serikali ya Zanzibar, imeelekeza baadhi ya masuala ya kuchunguza ikiwa ni pamoja na ushiriki wa wanawake, vijana na makundi yaliyo pembezoni, ukiukwaji wa haki za binadamu, ufikiaji wa vyombo vya habari vya umma kwa kuzingatia misingi ya usawa pamoja na kuwepo kwa takwimu za kijinsi. Tume imeelekeza wachunguzi wawezeshwe kutumia makala za rejea ikiwa ni pamoja na Sera ya Jinsia na Ujumuishi (Gender Policy and Inclusion).
Mwongozo wa Tume ya uchaguzi ya Jamhuri Ya Tanzania (NEC) haukugusa kabisa uchunguzi wa ushiriki wa wanawake na vijana na makundi ya pembezoni, wala ukiukwaji wa haki za binadamu. Tofauti hizi zinatokana na nini? Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ina Sera ya Jinsia inayoelekeza utendaji kazi yake ambapo NEC haina. Hii inamaanisha kwamba ripoti za wachunguzi wa uchaguzi za Zanzibar zitatuwezesha kupata taarifa za uchunguzi zitakazotupa uhalisia wa mwenendo wote wa uchaguzi na taarifa timilifu zaidi kama wachunguzi watazingatia mwongozo wa tume. Wachunguzi wa uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utategemea na utashi wa washiriki na uelewa wao wa masuala ya jinsia katika uchaguzi.
No comments: