Tunapokaribia saa za ukingoni, katika safari ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu, wale wote wanaotuomba tuwape dhamana ya kutuongoza aidha kama Mkuu wa Nchi (rais), wawakilishi katika vyombo mbalimbali vya uwakilishi ikiwa ni pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na nafasi za udiwani, wanaongeza kasi ya kampeni. Tofauti na chaguzi zilizopita, mwaka huu ushindani ni mkubwa kutokana na kuunganika kwa ngome ya upinzani iliyovutia baadhi ya waasisi wa chama tawala CCM.
Pamoja na kuwa na ushindani mkubwa, wagombea wote wamejikita katika ahadi zinazoashiria kutatua kero au matatizo ya kila siku ya Mtanzania. Afya, maji, barabara, umaskini, ajira n.k.
Cha kushangaza ni kwamba, katika ahadi hizi za wagombea wote wawili, usawa wa jinsia hauko kwenye vipaumbele vyao ingawaje wote wanahimiza wanawake wawapigie kura. Kinachokosekana katika hizi ahadi ni msimamo wa kiitikadi utakaoongoza sera elekezi kwa mipango kazi ya kutimiza hizi ahadi.
Ahadi zisizojikita katika itikadi au falsafa ya kuleta mabadiliko ya mifumo kandamizi haziwezi zikawezesha mabadiliko tunayotarajia kama wapiga kura hususani mifumo iliyowabagua wanawake katika ufikiaji, na kunufaika na matokeo ya maendeleo. Sisi tumeshuhudia kukua kwa uchumi ambao haukuwa linganishi. Ongezeko la shule ambazo hazijawezesha watoto wa kike kukabiliana na changamoto za mimba za utoto na ndoa za utoto. Ongezeko la huduma za afya ambazo hazikuenda sambamba na kukabiliana na vifo vya wanawake wanaoendeleza uzalishaji wa taifa wanapobeba mimba au kujifungua. Ongezeko la huduma za usalama ambazo hazilindi usalama wa mwanamke ndani ya nyumba. Kwa siku chache zilizobaki, wanaoomba kura watuambie itikadi inayoongoza vyama vyao na mikakati ya kubomoa mifumo kamdamizi.
No comments: