Mdahalo Wagombea Urais Chini ya Matarajio


Na Balozi Dr. Ahmed Kiwanuka.

Siku ya jumapili ya Oktoba 18, Shirika la utafiti la TWAWEZA liliendesha mdahalo wa wagombea nafasi ya Rais. Mdahalo huo ulihudhuriwa na wagombea karibu wote isipokuwa wangombea wawili ambao wamekuwa wakivutana mashati kwa kuwa na ushindani mkali wa kuvutia watu kuhudhuria mikutano yao. Wagombea hao Edward Ole Ngoyai Lowassa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na mwenzake Dr John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawakuoneka katika mdahalo huo.


Jambo hilo lilisababisha mdahalo kuwa chini ya matarajio ya wananchi wengi. Kutokuwepo ushiriki wa wagombea wa CCM na CHADEMA/UKAWA kulisababisha mdahalo huo kuwa wa vyama vidogo hivyo kuyeyusha mvuto wa mdahalo wenyewe.

Ingawa maoni yaliyojitokeza hayakuwa mazito si ya kupuuzwa. Kwa mfano, suala la mifuko ya hifadhi ya jamii, serikali lazima iwe na sheria moja tofauti na ilivyo sasa kwa kila mfuko wa hifadhi kuanzishwa kwa sharia yake jambo linalominya usawa kwa wananchi.


Suala lingine ni serikali kusimamia na kutengeneza sheria inayompa kila mwananchi uhuru wa kupata na kuchangia mfuko anaoupenda hasa kwa kuwa mifuko yote itakuwa na sheria moja. Mbali na mifuko ya hifadhi ya jamii, deni la taifa linaathari kubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa ujumla wanahitajika viongozi wenye uchungu na nchi kusimamia kikamilifu matumizi ambayo yatakuwa sio ya lazima na kuyaacha, iwekwe wazi kabisa uhusika wa Bunge katika usimamizi /udhibiti wa deni la Taifa. Na kuhusu amani ya nchi ni wajibu wa kila mtu kutambua kila raia analojukumu la kuilinda. Na hasa kwa wale wanaosimamia haki wawe ndio mstari wa mbele kuitoa haki ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Kukubali matokeo ya uchaguzi ambayo ni halali ni njia moja wapo ya kuilinda amani maana asiyekubali kushindwa si mshindani ila kwa njia zilizo za kweli.
Chaguzi zijazo ni vyema midahalo ikatiliwa mkazo maana inatoa nafasi kwa wagombea kuonesha uwezo, maarifa, mvuto kwa wakati mmoja kwa wapiga kura. Nafasi hiyo ikitumika vizuri ni mtaji tosha kwa wagombea pia enzi hizi za TEHAMA, midahalo ni alama muhimu ya kuimarisha demokrasia kwa vile sasa mambo yapo nje nje.

No comments:

Speak Your Mind

Powered By Blogger · Designed By Seo Blogger TemplatesPublished.. Blogger Templates